MAJIRA NA NYAKATI

MAJIRA NA NYAKATI YA SIKU YA LEO.
Siku ya NNE.
Lango la 25.
Mwezi ABIBU.
Mwaka wa 6 wa UKAMILIFU NA UTIMILIFU WA ISAYA 2:2-4 NA ISAYA 60.
(29 October 2016)

KUSIMAMISHA SIKU 7 ZA HATI MILIKI YA KITI CHA URITHI WA MUNGU KWA WATAKATIFU


Lango la 1 Shebati 5 SIKU YA KWANZA

WAKILI WA MUNGU KIZAZI CHA MUNGU
ELISHA ELIYA MIAKA1000


SHUKRANI
Tunamshukuru MUNGU leo siku ya kwanza, siku ya nuru, pia ni siku ya kwanza katika mwezi wa Ushindi katika mwaka huu wa tano. Tunamshukru MUNGU kwa neema ambayo ametupa kuwepo mahali hapa siku ya leo. Nina mambo matatu ya kumshukuru MUNGU kwa ajili ya mwezi uliopita:

1. Kupitia Eze. 36:26 MUNGU ametupa:
+ Kila kitu kuwa vipya, uumbaji mpya: Moyo, roho, na nafsi mpya, na viungo vipya, kila kitu ni kipya kabisa. Sura yako ni mpya, nywele zako ni mpya, macho yako ni mapya, kinywa chako ni kipya, mawazo yako ni mapya, matamanio ya moyo wako ni mapya kabisa.

Mwambie MUNGU kwamba nakushukuru kuwa umenikumbusha kwamba nilitakiwa nijifungie mahali ili nione kila kitu ni kipya. Mwambie MUNGU napokea kifua kipya, tumbo jipya, moyo mpya, kongosho mpya, maini mapya, damu mpya, mishipa mipya, mgongo mpya, mifupa mipya na umbile jipya, mahusiano mapya kabisa katika yangu na majirani, na ndugu zangu wa unabii wa kuolewa, kati yangu na kichwa, na kanisa, na watoto wangu, na kila mmoja anayenizunguka.

2. Efe 5:27 – Kanisa kufunuliwa kwa malango ya MUNGU
MUNGU amelifunua Kanisa kwa malango yake mwenyewe kwa malango ya Neno na ufahamu wake mwenyewe. Mwambie MUNGU nakushukuru kwa sababu kila mmoja ufahamu wake umekwenda juu; utii wa neno umekwenda juu; utakatifu umekwenda juu; na kumwamini MUNGU kumeongezeka. Lazima tumwambie MUNGU tunakushukuru kwa sababu kila mmoja amejitambua. Hakuna anayekwenda kumdai baba yake wa viungo vya ufunuo kwamba hujanipa urithi. Wote tunajua kuwa aliyetufunua ni MUNGU mwenyewe. Utaona jinsi anavyomimina vitu vizuri kwako. Jana nimepata fedha mara tu nilipotoka hapa, nilipopata nikajua na wengine watapata, maana urithi sasa ni kwa MUNGU mwenyewe. Asiwepo kabisa wa kumgombeza baba yake au ukoo, kwamba hawajakupa kihamba. Sasa hivi MUNGU mwenyewe ndiye anakupa kila kitu kwa sababu tumefunuliwa kwa malango yake yeye mwenyewe. Mwambie MUNGU nakushukuru kwa kuwa sasa nimekuelewa. Yale makunyanzi makunyanzi uliyokuwa unayaona ndani ya Kanisa hutayaona tena. Katika mwezi huu wa ushindi utaona kila mmoja ambacho kilikuwa kinamshinda sasa utaona anakiweza. Kuna madhaifu madhaifu yalikuwa yamebakia ndani yako sasa yatayeyuka yenyewe kwa sababu sasa umetambua.
3. Ukamilifu wa kiti cha urithi - 1Fal.9:1-5
Kila mmoja amshukuru MUNGU kwa sababu sasa umepewa kiti. Mahali ninapokuunganisha leo ni kupata Hati Miliki. Maana unaweza ukapewa kiti cha urithi lakini ukanyang’anywa. Leo tunasimamisha siku 7 za hati miliki. Kwanza tumshukuru MUNGU, maana hata Adamu1 alipewa kwa ukamilifu kabisa, lakini aponyang’anywa Hati Miliki akaambiwa ondoka. Leo unarejeshewa na hati miliki unapewa. Mshukuru MUNGU kwamba umenipa kiti cha urithi kwa ukamilifu na sasa unanikabidhi hati miliki. Hakuna atakayekuja kukuuliza umepewa na nani kwa kuwa umepewa na Mzee wa Siku ingawaje kerubi zamani aliichukua hii hati, tukafikiri tunamwabudu MUNGU kumbe ni kerubi, leo tumerejeshewa.

4. Kulipwa sawasawa na usafi wa mikono yako - Zab.18:20.
Mwambie MUNGU asante kwa sababu tumeanza kulipwa; kama unaona ulifanya mabaya, omba rehema na usimamishe toba ya MUNGU. Toba ya MUNGU ilileta uhuru kwa kila mmoja aliyeelewa, wakati mwingine MUNGU analeta neno lakini hatulifuatilii. Kupitia toba ya MUNGU kila mmoja aliwekwa huru, lakini ni mpaka Yule anayependa kuwa huru. Mwambie MUNGU nakushukuru kwa sababu ninalipwa sawasawa na usafi wa mikono yangu.

5. Shukrani kwa ajili ya vituo vyote na kuuleta uumbaji wote madhabahuni.

Kama kuna mlima ulichukua hati miliki ya mwenye haki tuulete hapa; Kama kuna ukoo au kabila ulichukua hati miliki yako warejeshe sasa hivi; Kama kuna mtume, au nabii au mwinjilisti alichukua nyota yako, arejeshe sasa hivi; hata kama ni mwalimu au nabii wa uongo. Kila mmoja aje nacho alichonacho ili aulizwe, je, hii ni ya kwako, au ni aje? Sasa hivi anarejesha, kama yupo aliyemuibia yeyote, anaanza kuulizwa na malaika, kwamba ni ya kwake au ameiba? Kama kuna aliyeiba afya yako anarejesha sasa hivi; kama ulikuwa na tanzi au umefungwa sasa aliyekuwa huru kwa niaba yako sasa afungwe. Ndiyo hapo tulipoingia sasa hivi ili yale yaliyo Isa 49:20 watoto hawa walikuwa wapi ulikuwa umenyang’anywa lakini sasa unarejeshewa.

Tunapozungumza Hati Miliki ya Kiti cha Urithi wa MUNGU tuna maanisha nini? Tunapozungumza kiti cha urithi, siyo hicho unachokalia. Tuna maana ya mahali ambapo MUNGU alikukusudia tangu mwanzo. Tuna maana ya:
+ Ile safu ambayo MUNGU alikukusudia;
+ Ile biashara ambayo MUNGU alikukusudia;
+ Ile familia ambayo MUNGU alikukusudia;
+ Ile familia ambayo MUNGU alikukusudia;
+ Lile agano ambalo MUNGU alikukusudia;
+ Ile kazi ambayo MUNGU alikukusudia;
+ Ule wajibu, ile nafasi ambayo MUNGU alikukusudia tangu mwanzo.

Hiyo nafasi ina gari, nyumba, mshahara na marupurupu, ina kila kitu ambacho unastahili kupata, kwa kuwa ni haki ambayo MUNGU alikukusudia tangu mwanzo. Kuna mahali MUNGU alikusudia uishi, kuna nafasi MUNGU alikusudia uwe nayo, na ina kila kitu ambacho unastahili kupata. Kila siku alfajiri MUNGU anatuma malaika kuleta kila kitu kinachotakiwa katika nafasi hiyo na mahali pale, kwa kila mmoja. Kwa ujumla, huyu Mzee wa Siku, hadaiwi chochote kwa yeyote; ila kuna waliokuwa wanavuruga. Kwa hiyo basi, tunapozungumza kiti cha urithi, ni wewe kupokea yote ambayo MUNGU aliyakusudia.

Kuna kitu kinaitwa Hati Miliki; unaweza ukawa wewe mwenye haki, uko mahali ambapo MUNGU alikukusudia. Lakini hakuna yeyote ambaye aliwahi kupata marupurupu, hasa mwenye haki, yanayofanana na kile ambacho MUNGU alikusudia. Hii ni kwa sababu Neno linasema “mateso ya mwenye haki ni mengi” ila MUNGU ni mponyaji, na amekuja kutuponya.

Mwenye haki yeyote hakuwahi kupata marupurupu sawasawa na nafasi ambayo MUNGU alimkusudia kwa sababu yalikuwa duniani. Hii ni kwa sababu yeye mwenyewe MUNGU alipoumba Mlima wake, alitolewa pale na kerubi. Hiyo ikawa limbuko kwa kila mtakatifu (mwenye haki) kusogezwa pembeni, mpaka alipokuja juzi kupitia Dan.7:22(a) wakatakatifu wakapewa hukumu, Dan.7:22(b) wakati ukawadia watakatifu kuumiliki ufalme. Kwa hiyo kuna kitu kinatangulia hapa, kama vile jana MUNGU alitangulia kusema kwamba sasa ni wakati wa kulipwa sawasawa na usafi wa mikono yako, halafu ndiyo (b) itokee. Ndipo wakati uwadie wa kumiliki, lakini ili umiliki, ni lazima upewe Hati Miliki.

Mlima wa BWANA
Hapa tunakuta kuna madini ya kila aina, lakini mhusika mwenyewe akawekwa pembeni, kwa hiyo limbuko lilianzia pale.

Bustani ya Edeni
Mahali ambapo nataka nipaweke wazi kwanza ni Mwa.2:15. Hapa MUNGU alisema nakupa bustani hii, uilime na uitunze. Hiki ni kiti amepewa, lakini katika kiti alichopewa kilikuwa na masharti. Kwa nini alimpa masharti? Alipewa masharti kwa sababu pale pembemeni palikuwepo na “Mti wa ujuzi wa Mema na Mabaya”. Kwa hiyo akasema hivi, “ili kiti hiki nilichokupa, cha kutunza bustani hii, kula vizuri, kunywa vizuri, kuishi vizuri, iwe hivyo, basi usishirikiane wala usichume matunda kwenye mti wa Ujuzi wa Mema na Mabaya”. Hii ni sawa sawa na jinsi ambavyo MUNGU anamwambia Sauli kupitia 1Sam.10:1-, kwamba nimekupaka mafuta uweze kuwa juu ya Israeli, uweze kuwaokoa katika shida za aina mbali mbali, lakini akamweleza na masharti. Anampa masharti kwa sababu tayari kuna mwingine anatafuta kumnyang’anya ile nafasi. Hiyo ilikuja kutokea kwa Sauli katika 1Sam.15 akapoteza ile nafasi kwa sababu hakufuatilia yale masharti.

Je, ni nini hasa ninachotaka kusema hapa? Bado niko hapa katika Dan.7:22, ni mstari wa ajabu kweli kwa sababu una vipengele viwili. Kuna kipengele cha kumiliki, lakini kwanza “hukumu ipite”. Ninachotaka kusema ni hiki: Ili Adamu1, katika Bustani ya Edeni, akae vizuri bila matatizo, ilikuwa ni lazima kwanza ile Mwa.2:8 ambayo ina “mti wa ujuzi wa mema na mabaya” ifutike kwanza. Hicho ndicho kinachofanyika kwenye Dan 7:22a. Lakini pia ilikuwa ni lazima Mwa.1:2 ambayo ina “giza, ukiwa na utupu (GUU) ifutike kwanza. Hapo ndipo angekaa vizuri. Kuna kitu nataka nieleze hapa, kwamba kwa nini MUNGU amekuja kueleza hapa kwenye Dan.7:22 kwa vipengele viwili; ni kwa sababu kuanzia mwanzo ameona kilichotokea kule nyuma. Hataki tena yale yaliyotokea kule mwanzoni yajirudie Kizazi hiki.

Kwa sababu Kizazi hiki tumerudi kule mwanzoni, inabidi hukumu ipite kwanza ndipo wakati uwadie wa kumiliki. Kwa hiyo basi nataka utambue, kwamba ni kweli kabisa MUNGU amekuwa akitamka katika siku zote 6 zilizopita, yaani vizazi vyote vine, sasa siku ya saba (7) imefika, anataka yale yote ambayo yangezuia usikalie vizuri kiti chako, yahukumiwe kwanza. Yakishahukumiwa hayo, utakalia kiti chako bila shida. 

Vitu mbali mbali ambavyo MUNGU alikuwa ametukusudia, lakini hati miliki ya vitu hivyo ilikuwa bado iko duniani.

1. Mwa.1:2 - siku ya 7 ya kustarehe.
Nikuulize wewe mwenye haki, tumeshafika siku ya Saba (7), Je, unaishi kwa kustarehe? Hapa kila mmoja nikimuuliza, ana lake la kuniambia. MUNGU anachotaka kufanya sasa, ni kuhukumu hayo yaliyokuwa yanakuzonga wakati umeshafika siku ya 7 ili usatrehe pande zote. Ndiyo maana ya mstari huu; amekuja ili atusaidie kwa sababu hataki tena tuishi kwa wasiwasi; hataki tena tucheze na tuimbe kama tulivyocheza siku ya 5, halafu ukirudi nyumbani unaanza kulia; Hilo hataki! Anataka iwe furaha ya milele! Kila anayekuona, akuone unachekacheka kila dakika. Kwa hiyo basi, jambo hilo lililokuwa linasababisha usichekecheke kila wakati, ndilo la kwanza kuhukumiwa leo hapa na Mzee wa Siku mwenyewe, ili kustareheshwa pande zote kuonekane. Mwenye uwezo wa kuhukumu hayo ni yeye mwenyewe.

Jambo moja niseme, Roho ya Matengenezo, Marejesho, upatanisho na kujenga, imetusaidia kutufikisha mpaka hapa kwa Mzee wa Siku. Maana bila hiyo tusingefika. Naomba mnielewe, kuna wanaofikiri nimeachana na Roho ya Eliya, hapana! Roho ya Eliya huwezi kuachana nayo, utafikaje kwa Mzee wa Siku bila Roho ya Eliya? Mnatakiwa mlielewe jambo hili kwamba, hilo ndilo daraja ambalo limetufikisha kwa Mzee wa Siku. Hilo ndilo daraja limetufanya tufike kwa Aliyetuma wote. Mnielewe vizuri ninachofundisha! Ila kuna vitu vingine, Roho ya Matengenezo, Marejesho, Upatanisho na Kujenga ilikuwa haiwezi mpaka aje Yeye mwenyewe Mzee wa Siku. Kwa sababu vitu vingine alivitamka yeye, kama alivitamka yeye, ni lazima yeye mwenyewe avifute. Ndiyo maana mimi nikampisha, nikasema naomba ufanye wewe mwenyewe.

Kitu cha kwanza kabisa ambacho ilikuwa lazima MUNGU aanze nacho ni hiki cha kusafisha siku ya saba. Benchmark (Kigezo) yetu iko kwenye Dan 7:22 ambayo ina a na b, kwamba  lazima hukumu ipite kwanza, hukumu ikipita ndipo wewe ukaliye kiti chako bila shida. Kwa hiyo, ina maana kwamba Hati Miliki ya Siku ya Saba ilikuwa bado ipo duniani. Ukitaka kujua kuwa hivyo ndivyo ilivyo, angalia mahudhurio ya hapa Kanisani siku ya 7 na siku ya 5. Ndiyo utajua kwamba hati miliki ya Siku ya 7 ilikuwa bado iko duniani.

Miezi hii sita ambayo nilikuwa nalipa mahari ya Kanisa, kama hamkujua ndiyo nilikuwa nalipa mahari ya Kanisa hivyo. Ndiyo maana mimi nilikaa kimya, wengi inaelekea hamkujua, leo ndiyo nasema. Hili liko katika msingi wa Neno, katika Mwa.29:19-27, angalia jinsi Yakobo alivyolipa mahari hapo. Ukisoma kwenye ile barua waliyotuletea utaona kulikuwa na miezi 6, halafu wakasema nilipe tena mahari nyingine. Nikamwambia, MUNGU wewe ulisema Kanisa mmoja, na mahari nimelipa kwa miezi sita. Nilisema huu mtihani ni wa kwangu, na kweli mawe na fimbo zote waliweka chini wakatulia. Mahari ikalipwa vizuri, hakuna fujo iliyotokea. Sasa kama nimelipa mahari kwa miezi sita tena vizuri kabisa, kuna kanisa wawili, si ni mmoja tu?

Nikasema, MUNGU, Yakobo alikosea kwa sababu hakuwa na sababu ya kuoa wake wawili. Ndiyo maana alikubali kulipa mahari mara mbili, nikasema mimi hapana. Nikasema Yakobo alikosea, yeye ndiye aliyekuwa msingi wa Kanisa Kiazazi cha Kwanza, cha Pili, na cha Tatu. Lakini katika Kizazi cha kwako, Kanisa ni mmoja, labda MUNGU uniambie kama umebadilika. Lakini umesema kwenye Mal.3:6 kwamba wewe siyo kigeugeu na sasa mimi nataka kanisa moja tu rohoni kwa kuwamimi BWANA sina kigeugeu. Nikasema torati ya Musa ndiyo iliyoruhusu kuwa na mke zaidi ya mmoja. Lakini YESU alipoulizwa alijibu kwamba ilikuwa ni kwa sababu ya ugumu wa mioyo ya wana wa Israeli. Lakini siyo kwa sababu wewe MUNGU uliruhusu. Mimi nimemkamata kwa neno. Ni kweli kabisa zamani waha walikuwa wanaoa wake wawili mpaka wanne. Lakini hicho kitu hakuna tena sasa hivi, kwa sababu mimi nimeokoka, siwezi kuwa na makanisa wawili.
Ninachotaka kusema hapa kwenye swala la kustareheshwa pande zote, na nikirejea pale Mwanzo juu ya Kanisa katika Bustani ya Edeni. Nikirudi pale kwa Adamu1 ambapo ilibidi afukuzwe katika Bustani ya Edeni, alinyang’anywa Hati Miliki kwa sababu ya msingi, limbuko, chanzo na kitovu kilichokuwepo katika Eze.28:15b. Hapa ndipo kulipokuwa na msingi wa kunyang’anywa Hati Miliki kwa wenye haki. Ndicho kilichotokea hapa katika Mwa.2:15 kwa sababu alikuwepo huyu “mti wa ujuzi wa mema na mabaya”. Kwa hiyo nimekuambia MUNGU ambacho anataka kufanya sasa hivi kwanza ni kuondoa kila mahali ambapo pana mti wa ujuzi wa mema na mabaya uliokuwa unasababisha wewe utoke kwenye ukamilifu wa kitu ulichopewa jana (28 Thebeti 5). MUNGU anachoka ni kwamba ule ukamilifu ulioupokea jana usiondoke tena. MUNGU anafuta kuanzia kule juu mpaka jana (28 Thebethi 5). Pamoja na kwamba ulikuwa umepewa ukamilifu, lakini mti wa ujuzi wa mema na mabaya ulikuwa bado upo. Sasa kwa kuwa ulikuwa bado upo, hii Dan.7:22(a) lazima kwanza ifanye kazi ya kuondoa mti wa ujuzi wa mema na mabaya.

Hii ina maana Adeni na Edeni ilikuwa bado ni unabii. Ndiyo sasa tunapewa, lakini kwanza mti wa ujuzi wa mema na mabaya, uondoke. Kumbuka nimesema kwamba nikisema Adeni nina maana ya ufahamu wa MUNGU. Nikisema Edeni, nina maana ya nafsi ya mkamilifu. Kwa hiyo ina maana kwamba mpaka leo miliki ya Adeni ulipewa jana lakini bado pembeni kulikuwepo na ambaye angekunyang’anya. Nafsi yako mwenyewe (Edeni) mpaka sasa hivi, ilikuwa bado ina mti wa ujuzi wa mema na mabaya.

Ambacho Mzee wa Siku amekuja kutusaidia, ni kuhukumu hicho ambacho kingesababisha unyang’anywe ule ukamilifu wa kiti cha urithi. Mpaka leo pamoja na ukombozi wa Kanisa ambao umekuwa ukifanyika, lakini MUNGU alikuwa bado hajaketi sawasawa Adeni. Kanisa nalo lilikuwa halijaketi sawasawa Edeni. Ila jana kiti umekabidhiwa kwa ukamilifu, lakini sasa MUNGU leo ameamka na Hati Miliki ili usiondolewe tena.

Unapozungumzia Adeni, una maana ya ufahamu wa MUNGU ambao bado ulikuwa umesongwa na elimu ya dunia ya saikolojia, falsafa na thiolojia. Unapozungumzia Edeni, unazungumzia nafsi yako wewe mwenyewe mkamilifu, ambayo nayo ilikuwa bado imesongwa na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.

Maisha yako yote wewe ambaye unamfuata MUNGU wa kweli yako Adeni na Edeni. Kwa sababu ukizungumzia madini ambayo yanatengeneza kila kitu, yako Adeni (mlima wa BWANA). Ukizungumza mashamba, ukazungumza ufahamu wa MUNGU, pumzi ya MUNGU, uhai wa MUNGU, ukazungumza kila kitu ambacho mimi na wewe tunatakiwa tuwe nacho kiko Edeni (yaani kwenye nafsi yako wewe mwenyewe). Ambayo inategemea umeweka ufahamu wa aina gani, maisha yote yapo hapo. Lakini bado hicho kiti cha kuyarithi haya, ambacho jana umepewa, anytime (wakati wowote) kama huu msitari wa Dan.7:22 usingefanya kazi, ungenyang’anywa, kama ilivyotokea kwa Adamu1 na wengine wote waliofuata.

Maeneo mengine ambayo MUNGU alitupa lakini tukawa tunanyang’anywa kwa sababu MUNGU naye alisogezwa pembeni:

1. Ibrahimu Mwa.13:10 – Roho ya Lutu
Neno linasema hapo kwamba “Lutu akainua macho yake, akaliona bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji, kabla BWANA hajaharibu Sodoma na Gomora, lilikuwa kama Bustani ya BWANA, kama nchi ya Misri hapo unapokwenda soari”. Mpaka leo bonde hilo la Yordani bado liko kwa watoto wa Lutu. Lutu siyo jina, bali Lutu ni roho. Umeanza vizuri biashara, kuna mnayefanya naye biashara, yeye anainuka wewe unashuka. Ibrahimu alipewa kiti cha urithi lakini Lutu akachukua Hati Miliki mpaka leo. Kwa hiyo ina maana kwamba jambo hilo lazima lihukumiwe na Mzee wa Siku, halafu baada ya hukumu Ibrahimu ambaye ndiye mwenye ahadi atapata. Hiyo ndiyo kazi tunayotakiwa kufanya.

Jambo hilo linaonekana hivi, bustani ya Edeni MUNGU alimpa Adamu1 mambo yakaharibika. Akachungulia akamuona Ibrahimu, alipompa Ibrahimu, Lutu akachukua. Ili ujue kwa nini Lutu alichukua, inatakiwa uanzie nyuma katika Mwa.12:4. Hapo ndipo mambo yalikoanza kuharibika kwa Ibrahimu.

(a) Katika Mwa.15:1-7 Ibrahimu alipewa kiti cha kurithi watoto. Ameahidiwa kabisa kwamba nitakupa mototo wa kutoka kwenye kiuno chako wewe mwenyewe atakayekurithi. Lakini katika Mwa.16:1 anaibiwa; na katika Mwa.17:18-20 yeye mwenyewe vitu vyote vizuri alimkabidhiwa Ishmaeli. Mpaka leo havijawahi kurudi. Ukienda uarabuni magari na ndege za waaarabu ni nzuri kuliko za wazungu wenyewe wanaotengeneza. Hapa tunazungumza Hati Miliki.

Unapewa kabisa kwa ukamilifu lakini unanyang’anywa bila kujua. Sasa tumefika kwenye siku 7 za kuhakikisha kwamba kile kitu ulichopewa kwa ukamilifu, usinyang’anywe. Nimekwisha kuambia kwamba tunapoongea juu ya kiti, siyo hicho ulichokalia bali ni yale marupurupu ambayo yako kwenye ile nafasi ambayo MUNGU amekupa kwenye: agano, familia, biashara, kazi, shamba, kila mahali. Kuna nafasi MUNGU amekupa, na kuna marupurupu hapo. Lakini kwa mwenye haki alikuwa hapati, sasa ni wakati wa kupata.

(b) Katika Mwa.27 Isaka (mwana wa ahadi) alipata upofu wakati wa kugawa urithi, halafu akagombanisha watoto. Alipogawa urithi akamwambia na mwingine aende hapo hapo, lakini apate kwa upanga. Kwa hiyo ina maana basi huyu mwenye haki hajaruhusiwa kuona mpaka leo. Kwa hiyo lazima arejeshewe kuona, asiporejeshewa itakuwa vigumu kwake kukitumia kiti ipaswavyo. Hakuna kitu hakipo kwenye Neno, lakini mpaka MUNGU akuambie.

Kinacholeta shida mpaka wengine duniani wanaichukia Siloamu, ni kwa sababu tunakwenda na MUNGU anayetuambia sasa tumefika hapa, sasa hivi tumefika hapa, n.k.. Hicho ndicho kinachowafanya wengine waichukie Siloamu. Gari la Siloamu halina “reverse” (halina gia ya kurudi nyuma), linakwenda mbele tu. Hicho ndicho wanachochukia, kwamba nisije (Wakili) nikawahamisha kituo. Mimi sifundishi ambacho MUNGU hajasema. Kama una akili utaona kabisa kwamba leo tulikuwa hapa, kesho tumekwenda mbele, na keshokutwa tumekwenda mbele zaidi. Sasa nimekosea wapi? Siwezi kusimama madhabahuni bila MUNGU kuniambia leo tumefika hapa. Mimi mpaka sasa hivi, mama yangu wa viungo vya ufunuo sijui anaishi wapi, ingawa anaishi mji huu huu. Hii ni kwa sababu akili yangu yote ni mbinguni tu. Mimi siwazii kitu kingine. Ukiniambia nikupeleke mahali ambapo mama yangu yupo, siwezi kwa sababu sipajui. Nimemkabidhi kwa MUNGU alelewe na MUNGU. Mimi akili yangu inawaza vitu vya mbinguni tu.

Siwezi kuja hapa kukufundisha vitu ambavyo MUNGU hajaniambia, hata siku moja. Hicho ndicho kinachoudhi dunia. Sina kosa lingine, kosa langu ni kutembea na MUNGU; kama ni kosa. Kwa hiyo wewe mwenye haki leo upewe macho ili uone fursa. Kati ya vitu vilivyoleta shida kwa Isaka ilikuwa ni kupewa upofu. Ukiangalia hapa mjini wanaotoka Ulaya, Amerika, Asia n.k. wanapokuja hapa, hawaji na fedha. Anakuja tu na akili yake, fedha anapata hapa hapa. Anaanza kujenga kiwanda kwa fedha ya hapa hapa. Hii ni kwa sababu kuona kulitoka kwa Isaka kukaenda duniani. Atatoka Amerika, au Ulaya, mkishamaliza kusaini mkataba, anasema ngoja sasa nikachukue fedha China. Hii ni kwa sababu ya kuona, lakini sasa umepewa kuona kwa Damu ya MUNGU mwenyewe. 

(c) Mwa.26:1-12 - Isaka
Hapa Isaka alikwenda kufukua visima vya baba yake Ibrahimu lakini kuna jamaa walimfukuza. Akachimba cha kwanza wakamfukuza, akachimba cha pili, wakasema siyo cha kwako, mpaka cha tatu, ingawa hata cha kwanza na cha pili ni cha kwake. Kisima kile hakijawahi kufukuliwa hata siku moja. Sasa imefika wakati kisima kile kifukuliwe, kwa sababu ni chake na ni chako wewe. Sasa Hati Miliki ilikuwa bado iko duniani.
Ushuhuda
Kuna dada mmoja alikuwa na kampuni kubwa sana ya mawasiliano. Alikuwa akienda kwa wafanyabiashara wenzake, wanamwambia wewe haupo kwenye chama chetu. Nani amekupa kampuni kubwa namna hii? Wakimwambia hivyo anashindwa kuwaelewa wana maana gani. Kila walipokutana, mikutano yao inafanyika kwenye hoteli kubwa kubwa hapa mjini, wanasema wewe, nani amekupa kampuni kubwa namna hii? Mbona hatujawahi kukuona kwenye chama chetu? Anajiuliza chama gani hicho? Siku nyingine anakwenda, wanaanza kuuliza, wewe una kampuni kubwa hivi? Mpaka akawa ana changanyikiwa. Lakini sasa simuoni hapa, sasa sijui labda na yeye amekwenda kwenye chama hicho? Ninachotaka kusema hapa ni kwamba Hati Miliki ya Kiti cha Urithi ilikuwa bado iko duniani. Wakati nikiwa chuo kikuu, kuna watumishi Fulani walokole, ilikuwa mkimaliza shule walikuwa wanatengeneza chai fulani waliyokuwa wanaita ‘coffee house’. Hawajawahi kumuonyesha fomula hata mmoja, yaani ina harufu ya aina yake, na ilikuwa inapikwa siku hiyo tu. Kwa hiyo ilikuwa kama kuna walokole wanaomaliza, siku hiyo ikifika mnakimbia kwenda kunywa hiyo chai yenye harufu ya aina yake ambayo hawajawahi kuitoa fomula. Anayesinzia mwambie leo kuna jambo la aina ya pekee atapitwa.



2. Kut.14:15-29 – Musa, Zamu ya Nne
Huwa kuna zamu nne: Zamu ya kwanza Saa 1-3; Zamu ya pili Saa 3-6; Zamu ya tatu Saa 6-9; Zamu ya nne 9-12. Katika zamu ya nne ndipo kulipotokea ushindi kwa waisraeli. Hiyo Hati Miliki yake hatujawahi kupewa. Wengi hapa ni mashahidi kwamba ikifika saa hiyo huwa ukandamizwa, kuamka inakuwa shida kabisa. Sababu ni kwamba huo ndio muda ambao malaika wanaachiliwa kuleta baraka zako za siku. Sasa kuna wale jamaa wanaoamka kwenda kuswali, ndio wanowadaka hao malaika. Ukitoka kuswali huruhusiwi kwenda kusinzia, kuna sharti kwamba ukienda kusinzia unanyang’anywa Baraka ulizopata pale. Lakini wakati huo wanaoitwa wakristo, wanakoroma. Sasa hiyo Hati Miliki ya zamu ya nne lazima uipate leo. Ili uwe macho mwambie MUNGU leo nataka vitu vizuri. Kuna vitu vilikuwa bado hatujapewa, na MUNGU ameamua kuongea namna hii kwa sababu sasa ni wakati wa kupokea Hati Miliki. Unajua unaweza ukajenga ghorofa lakini kwa kuwa Hati Miliki ni ya mwingine akaja akabomoa. Hamna kitu kinafanyika kwenye uumbaji uliofunuliwa ambacho hakianzii rohoni.

Tumepewa ibada katika Roho na Kweli lakini lazima tupewe Hati Miliki yake. Kuna vitu ambavyo itabidi MUNGU ahukumu ndipo hiyo Hati Miliki upewe, halafu hivyo vitu visiibiwe tena. Angalia neno linavyosema katika Mdo 19:35, “… na karani wa mji alipokwisha kuwatuliza watu, akasema, enyi wanaume wa Efeso, ni mtu gani asiyejua ya kuwa, mji wa Efeso ni mtunzaji wa hekalu la Artemi aliye mkuu, na wa kitu kile kilichoanguka kutoka mbinguni?” Anasema kwamba kitabu cha Neno kilipotoka mbinguni kiliangukia Efeso, na kwamba hakuna asiyejua hilo. Hivi unafikiri, kama siyo MUNGU unaweza ukawanyang’anya wale? Na MUNGU aliruhusu, maana anasema hili neno limepitishwa kwenye tanuru la moto mara 7, likahakikishwa kwamba ni kweli. Jamaa wamesimama wakasema hakuna asiyejua duniani, kwamba kile kitu kilichoanguka kutoka juu kinatunzwa Efeso kwa wayunani. Wayunani wana shirika linaloitwa Logos. Logos ni andiko halafu ni torati.

Ushuhuda
Alikuja dada mmoja hapa anakaa Ubelgiji, akasikia nasema lile neno Adeni, akasema Edeni nakubali, lakini siyo Adeni. Nikamuuliza kwa nini? Akasema nimerudi Ubelgiji, nilimuuliza mzee mmoja ana zaidi ya miaka 75 akasema hajawahi kuliona. Ninamwamini Yule kwa sababu wale ndio waliopokea kitabu.

Umeelewa kwamba kuna Hati Miliki ambazo zilikuwa bado mahali ambazo leo unapewa, lakini lazima MUNGU apitishe kwanza hukumu, ndipo wewe ukae bila kunyang’anywa tena. Kwa sababu ni wakati wa mwenye haki kuwa na kampuni kubwa. Wasije wakasema mbona aliyeokoka ana kampuni kubwa? Wasije wakasema mbona mwafrika ana shamba hili kubwa? Wasije wakasema mbona uko katikati ya watu, nawe ulitakiwa uwe Mabwe Pande? Kuna mambo ambayo MUNGU itabidi atusaidie kuyafuta ili tupokee kiti cha urithi.

3. Swala la majira na nyakati
Hivi kuna ambaye hajui kwamba kitabu kinasema kuwa wiki ina siku saba? Mwezi una wiki nne. Kila mmoja duniani anajua. Lakini kwa nini wanang’ang’ania siku 29, 30, na 31? Ina maana kuna mahali kuna Hati Miliki ya Majira na Nyakati za MUNGU, ambayo ni lazima MUNGU atupatie.

Hati Miliki ya Majira na Nyakati za MUNGU iko duniani. Katika Mhu.9:11-12 Neno linasema “11Nikarudi, na kuona chini ya jua, ya kwamba si wenye mbio washindao katika michezo, wala si walio hodari washindao vitani, wala si wenye hekima wapatao chakula, wala si watu wa ufahamu wapatao mali, wala wenye ustadi wapatao upendeleo; lakini wakati na bahati huwapata wote. 12Maana mwanadamu naye hajui wakati wake; kama samaki wanaokamtwa katika nyavu mbaya, na mfano wa ndege wanaonaswa mtegoni, kadhalika wanadamu wananaswa katika wakati mbaya, unapowaangukia kwa ghafla”.

Wakati mbaya: Kile kitendo cha kusema siku inaanza saa sita usiku wakati huwezi kwenda kazini, na mkakubali kwamba kweli siku inaanza saa sita, kwa kweli ni wakati mbaya. Ina maana, kuna mwenye Hati Miliki ya kukamata akili za dunia nzima, zikakubaliana kitu ambacho siyo kweli. Anasema jioni ni saa sita mchana, na asubuhi ni saa saba mchana, na wote tukakubaliana dunia nzima, hakuna anayeuliza swali. Halafu unasema ni kawaida, wasomi wote, maprofesa wamekubali, vyuo vikuuu vyote vimekubali. Hata mitume, manabii, wainjilisti wote wamekubali, walimu na wachungaji wote wamekubali. Halafu useme ni kawaida hiyo? Kuna Hati Miliki ya Majira na Nyakati za MUNGU mahali inayokataa kwamba asubuhi siyo saa moja, na jioni siyo saa kumi na mbili. Nadhani umeshaona kwa nini Siloamu inawindwa. Siyo kwa sababu tuna makosa; na mimi Miaka1000 sina kosa lolote. Kosa langu ni kusimamia haya ambayo Eliya AD2 alikuja nayo. Kwa sababu Eliya AD2 alisema kwamba tunahama vituo, na mimi nawahamisha vituo kila siku. Kosa langu ni kuwahamisha vituo kila siku, lakini huo ndio msingi wa Kanisa.

4. Kupakwa mafuta ya kukamilisha Kanisa bila hati miliki. Nimeanza kwa kusema hakuna mwenye haki ambaye alipewa nafasi na akawa na hati miliki, hakuna hata mmoja. Ndiyo maana, huwa nasema hakuna mwenye kosa. Je, inawezekana hamnielewi nina maana gani? Huwa nasema hivi, katika mtikisiko huu uliopita hakuna mwenye kosa. Huwa nasema kwamba, mnagombana bila sababu. Nina maana hiyo, kwamba hakuna yeyote mwenye haki aliwahi kupewa safu, akapewa na Hati Miliki ya safu yake. Hakuna hata mmoja. Kwa hiyo hakuna sababu ya kugombana kwa sababu hakuna mwenye kosa. Makosa tumeyakuta sisi wote, kuanzia mlimani, hakuna mwenye kosa. Mimi huwezi ukanikuta namtukana yeyote, kwa sababu nafahamu hivyo. Ndiyo maana nilimjibu kijana mmoja ambaye alisema kwamba mimi huwa na rahisisha mambo, sirahisishi, bali naelewa. Nikawaambia kwamba mimi nimejichimbia kwenye toba kwa sababu najua bila MUNGU haiwezekani. Kwa sababu hiyo:
+ sijawahi kumlaumu hata mmoja;
+ Sijawahi kumhukumu hata mmoja; kwa sababu hakuna hata mwenye haki mmoja aliyewahi kupewa Hati Miliki ya safu yake.
Leo mfunguke na atakayesikia kanda hii, afunguke. Hapa ni MUNGU tu ndiye anaweza kutusaidia.

Ushuhuda
Kuna wakati nilikuwa Uholanzi, wakatangaza nafasi za ukamishina wa European Union. Kuna mlokole mmoja akapata nafasi ya kuwa Kamishina wa ‘Human Rights’. Wakawa wanamhoji kwenye TV, kwamba wewe tumepata habari ni mlokole, na umeshakuwa Kamishina wa Human Rights, tuhakikishie kwamba utalinda haki za binadamu wakati wewe ni mlokole? Maana tunajua kwamba kuna haki zingine za binadamu ambazo walokole hamkubaliani nazo.
Aliikosa hiyo nafasi kwa sababu ni mlokole, lakini digrii zote anazo, lakini kwa sababu hawezi kuwaruhusu wazini barabarani, akakosa. Hii ni kwa sababu hakuna mwenye haki aliyewahi kupewa safu yake akapewa na hati Miliki yake. Ndiyo maana mimi niko kimya, naongea tu nikiwa madhabahuni. Maana nafahamu, ila nashukuru Mzee wa Siku amekuja. Kwa sababu Mzee wa Siku amekuja, na vitu vyote aliviumba yeye, sina shaka tena. Mimi ninachofurahi, ni kwamba tumefika mahali hapo, kwamba tumefika kwa Mzee wa Siku, Aliyetuma wote. Ana uwezo wa kurekebisha kila kitu. Kwa hiyo kama ulikuwa una huzuni, usiwe na huzuni tena. Huyu Mzee wa Siku atarekebisha kila kitu. Huna sababu kabisa ya kumwandikia mwingine meseji isiyofaa, maana siyo yeye; ilikuwa ni Hati Miliki ambayo iko duniani. Huna sababu kabisa ya kumchukia mwingine. Ila katika hizi siku 7 sasa ukazane, mwambie MUNGU nakushukru kwa kuwa umenipa ukamilifu wa kiti cha urithi, naomba na hati miliki yake. Kwa kuwa ni yeye, na anakupenda atakupa, ndiyo maana amekuvusha.  



No comments:

Post a Comment