KUSIMAMISHA MAJIRA NA NYAKATI ZA KUISHI KAMA WAKILI WA MUNGU ANAVYOISHI
MIAKA1000 YA KUTAWALA NA KRISTO
WAKILI WA MUNGU, KIZAZI CHA MUNGU
SHUKRANI
Leo ni siku ya majira na nyakati, tuko katikati ya wiki ya kutafakari ufahamu wa MUNGU kabla ya wazo la kuumbwa kwa kerubi. Kwa hiyo kama ulikuwa umekamatwa na ufahamu wa dunia leo lazima uvuke; kama kuna namna ambayo ufahamu wa dunia ulikuwa umekukamata kabisa leo lazima utoke.
Leo tunaongozwa na Efe.1:18 neno linasema “Macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo”. MUNGU anaposema macho ya mioyo yenu yatiwe nuru maana yake upate ufahamu wa neno la MUNGU. Sisi hatuoni kwa kutumia macho haya, bali tunaona kwa kupitia ufahamu.
Ushuhuda
Jana nilipokuwa nikiwa hapa madhabahuni, sijui ni wangapi waliona, wakati nanyuyiza mafuta kwenye sadaka. Kuna jamaa mmoja, pandikizi (giant), alikuja kunivamia na silaha, lakini alikuwa haonekani kwa macho ya viungo vya ufunuo. Alipofika karibu na Joshua Eluli alidondoka chini, lakini kwa kuwa alikuwa rohoni, Joshua Eluli hakumuona. Mimi nilipomuona nilistuka kwa sababu alikuwa pandikizi hasa. Kile chombo cha mafuta nilichokuwa nimeshika kilitikisika, lakini niligundua kuwa ninyi hamkuona. Ndiyo maana jana nilipokuwa nafundisha kulikuwa na milipuko, kwa sababu kulikuwana mapandikizi mengi yamevamia ibada kupinga neno la jana.
MUNGU anachotaka leo ni Macho ya mioyo yenu, yaani macho ya kila mmoja rohoni yatiwe nuru, ufahamu wa neno la MUNGU ujae ndani yetu. Ina maana mpaka tumefika hapa tulikuwa bado tuna ufahamu wa huko duniani, sasa kwa kuwa tumefika hapa lazima kila mmoja avuke.
Nani ambaye jicho linauma au linawasha sana? Ni jicho lipi linalouma? Hiyo ni ishara ya ufahamu. Tunapozungumza ufahamu, elimu yote uliyosoma shuleni iko kwenye macho yako. Neno unalolipokea hapa linatakiwa litunzwe kwenye jicho la kulia. Masomo yote uliyosoma kuanzia chekechea mpaka chuo kikuu, yako kwenye jicho la kushoto.
Tunachotaka sasa hivi kinachotawala iwe ni ufahamu wa neno. Ukitawaliwa na ufahamu wa neno utaona mambo ya rohoni.
Nataka umwambie MUNGU nina kushukuru, leo nikitoka hapa upofu wa rohoni basi, maana tulikuwa vipofu mpaka MUNGU akasema “nani aliye kipofu kama mtumishi wangu?” Siyo kwamba hana macho ya viungo vya ufunuo, hapana, anayo, ila haoni mambo ya rohoni. Kwa hiyo nataka tumshukuru MUNGU kwamba leo tukitoka hapa kila mmoja atakuwa anaona rohoni vizuri kabisa.
Kinachosababisha tubishane kanisani ni swala la Ufahamu. Kama wote tukifunguka tukaona, kila mmoja atagundua kuwa Miaka1000 hajawahi kukosea mahali popote. Si rahisi, kusimama mbele ya Kanisa na taifa ukasema kuwa “mimi sijawahi kuthubutu hata siku moja kusimama madhabahuni kutamka kitu ambacho MUNGU hajaniambia”. Kama huna macho ya rohoni, kwa kauli hii, utaona kama ninajikweza. Lakini sivyo hivyo, ndiyo maana leo, macho ya mioyo yetu yatiwe nuru! Kila mmoja leo atafunguka na kuona. Labda kama hutaki, ila kama unataka kila mmoja leo macho yake lazima yafunguke aone; ili ujue kwamba hujapotea.
Mimi sikuacha kazi, elimu yangu, na cheo kuja kukupoteza wewe. Yaani niambatane na kanisa na watoto kuja kukupoteza wewe? Si, kila mmoja atashangaa? Nataka tumshukuru MUNGU kwamba macho ya moyoni ya kila mmoja leo yatatiwa nuru. Ili ufahamu mwingine wowote uliokuwa unataka kukutoa mahali pa zuri uondoke kwa Damu ya MUNGU mwenyewe.
1Nya.11:1-2
Hapa imefunuliwa kwamba Kanisa la Kizazi cha Pili, lilimfuata Daudi, likamwambia hivi: “Hata wakati Sauli alipokuwa kwenye viungo vya ufunuo, ulikuwa unatutoa na kutuingiza. Leo tunatambua kwamba itakuwa zaidi, tutaambatana na wewe kuanzia leo; tutakuwa nyama katika nyama zako, na mifupa katika mifupa yako”.
Leo nataka utafakari, kwa nini Eliya AD2, akiwa kwenye viungo vyake vya ufunuo, akimaliza tu kufundisha, nilikuwa nasimama kufundisha yale yale? Ilikuwa hivyo ili kila mmoja atambue kwamba “huyu ndiye anayewaingiza na kuwatoa katika majira ya vizazi vyote”. Hii ndiyo sababu siku moja aliniuliza, tukiwa wawili, kwamba, tafadhali niambie, mimi ni nani? Nikasema, wewe ni kati ya wenye uhai wa nne! Akanyamaza. Alitaka ajue kama ninamfahamu; yaani alitakaajue kama macho yangu yametiwa nuru.
Nataka na wewe leo, utambue kwamba mimi nimesimamishwa mbele yenu kama maabara. Maabara ni mahali ambapo unafanyia vipimo vyote na kuthibitisha kwamba hiki ni sawa na hiki siyo sawa; kwamba MUNGU anataka hiki na hataki hiki. Nataka umwambie MUNGU kwamba leo, aidha niambatane na huyu anayesimama mbele yangu au niachane naye. Kwa sababu nimegundua kama ni wa kweli au siyo wa kweli. Ndiyo maana nimesema kwamba macho yako lazima yatiwe nuru. Mwambie MUNGU, nifungue macho leo ili huyu anayesimama mbele yangu nimfahamu kama ni yeye au siyo yeye. Hii ni muhimu sana; kitabu kinaturuhusu kuzipima roho. Nataka kila mmoja hapa, MUNGU afungue macho yake ya rohoni; na wewe mwambie MUNGU nifungue macho kwani nataka nijue kama ni yeye au siye. Ni muhimu sana MUNGU akufungue macho ili uone ufahamu ili usije ukashawishiwa na yeyote. Lakini pia unatakiwa uwe na ufahamu, kwamba, hivi huyu ni nani anayejifunua namna hii? Mwambie MUNGU nakushukuru kwa sababu leo ni siku ya kufunguliwa macho; na uandae sadaka yako kwa ajili ya kufungua macho yako ya rohoni.
Kuinua sadaka ya kufungua macho ya rohoni ya Kanisa
Leo tunatoa sadaka ya Efe.1:18, ikiwa ni kwa ajili ya kufungua macho ya kila mmoja. Hivyo unapotoa sadaka yako, mwambie MUNGU naomba leo unifungue macho ya rohoni ili nipate kuona kama nitafika salama au jamaa atatupoteza? Nataka kila mmoja afunguke macho.
Elimu yote kwenye macho yako iliyokuwa inakuzuia usimuone MUNGU, ikae juu ya sadaka ili iteketee pamoja na sadaka; Ile elimu ya ukoo, kabila, lugha, na jamaa, iliyokuwa inasababisha usimuone MUNGU ikae hapa ili iteketee pamoja na sadaka; Elimu yote ya shule uliyosoma tangu chekechea mpaka chuo kikuu iliyokuwa inakuzuia usimuone MUNGU, ikae hapa ili iteketee pamoja na sadaka.
Ushuhuda
Ninamshukuru MUNGU kwamba Kuhani Jambojipya yupo hapa leo. Ninakumbuka siku moja Eliya AD2 aliniambia, kuhusu Jambojipya, kwamba, “Miaka1000, umkumbuke huyu kuhani kwenye ufalme wako”. Siku ile hakuna aliyejua maana yake. Hakuna aliyeelewa Eliya AD2 alimaanisha nini. Yeye mwenyewe ndiye aliyekuwa anajua. Kuhani Jambojipya ana neema moja, kwamba nyumbani kwake kuna muonaji; ambaye humwambia, baba mbona umekata tamaa wakati uliambiwa hivi?
· Mwingine yeyote aliyekuwa amepotezwa leo arejee
· Mwingine yeyote aliyekuwa amepotezwa, au kudanganywa, leo mlango umefunguka arejee kwa damu ya MUNGU mwenyewe!
· Ndiyo maana MUNGU ameniambia nijifunue moja mpaka mwisho huku macho yenu yakiwa yametiwa nuru, ili mseme ndiyo au hapana, ingawaje haturuhusiwi kupiga kura. Mimi sitakuruhusu useme ndiyo au hapana, ila mwambie MUNGU nimekubali.
USHUHUDA WA MAISHA YANGU
Leo MUNGU ameniambia nitoe ushuhuda wa maisha yangu ili yule ambaye atakubali kuishi hivyo, aweze kufuatana na MUNGU, na yule ambaye hawezi kuishi hivyo ajue hawezi kufuatana na MUNGU.
MIAKA 1000 YA KUTAWALA NA KRISTO. Wakili wa MUNGU -KIZAZI CHA MUNGU |
1. Sifanyi chochote bila msingi wa neno, Kol.3:17.
Neno linasema kwamba “kwa kila neno au tendo, fanyeni yote kwa Neno”. Naomba unichunguze leo kama ulikuwa hujawahi kunichunguza, siwezi nikakupa ushauri wowote bila msingi wa neno.
· Siwezi nikakupa ushauri kama sijui neno linasemaje.
· Siwezi kufanya chochote kama sijui neno linasemaje.
· Siwezi nikaenda mahali popote kama sina Neno la kuendea mahali pale
· Siwezi nikaanza biashara yeyote wala nikafanya chochote kama MUNGU hajasema, hivyo ndivyo nilivyo.
Nimewashuhudia hata katika swala hili tulilokuwa tunapita, wakubwa wengi nimekaa nao, serikalini wengine nimesoma nao, ningeweza kwenda kwao kwa msaada, lakini sikufanya hivyo. Sikuthubutu kwa sababu pia naelewa kuwa neno katika Yer.17:5-8 “amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, amfanyaye kuwa kinga yake, na moyoni mwake amemuacha BWANA. Maana atakuwa kama fukara nyikani, hataona yatakapotokea mema; bali atakaa jangwani palipo ukame, katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, ambaye BWANA ni tumanini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, uenezao mizizi yake karibu na mto; hautaona hofu wakati wa hari ujapo, bali jani lake litakuwa bichi; wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, wala hautaacha kuzaa matunda”.
MUNGU ameruhusu hili swala litokee ili na ninyi mjifunze.
· Niko hivyo! Muulize kanisa, uliza watoto.
· Sifanyi chochote, siendi popote bila mstari wa Neno.
· Sifanyi chochote bila msingi wa Neno
Ukiona nimevaa hivi ujue kuna msingi wa neno. Mavazi yangu yote yanafanana kwa sababu mimi moyo wangu haubadiliki.
Nilikuwa na sababu za kuondoka hapa (yaani kujenga hema ya kuabudia mahali pengine), lakini msingi wa Neno unasema nilipakwa mafuta hapa madhabahuni. Pia mnafahamu kwamba wenye haki wote hawapendi ugomvi; ugomvi ukianza huwa wanaondoka. Lakini msingi wa Neno unasema nimepakwa mafuta nikiwa hapa madhabahuni; nikaambiwa kwamba, nakuachia kundi hili ulikamailishe.
Sasa ningeondoka, nani mwingine nitamuachia kundi hili alikamilishe? Mpaka yule aliyenipaka mafuta aseme. Na sasa yuko huku ndani. Najua nikisema hivi hamfahamu kama yuko humu ndani yangu. Hilo ni la kwanza, na ndiyo maana sithubutu kufanya jambo lolote bila msingi wa Neno. Katika Yn.1:1-5 Neno linasema hakuna kilichofanyika bila neno. Wewe unayefanya chochote bila msingi wa Neno huwezi kufanikiwa, hata ukifanikiwa ni kwa muda mfupi kwa sababu ukiona umefanikiwa leo, kesho kitaharibika.
MUNGU alishasema katika Yer.1:12 kwamba yeye huliangalia neno lake ili apate kulitimiza. Sasa nikiangalia elimu ya dunia, mnafikiri itakuwaje? Si nitafeli? Au wewe ukiangalia elimu ndipo ufanye, lazima utafeli. Nichunguze unipendavyo utanikuta niko hapo.
2. Rum.12:19-21 Mimi silipi kisasi.
Katika maisha yangu yote silipizi kisasi na haitatokea, kwa sababu neno la MUNGU linasema usilipe kisasi , maana hicho ni chake. Lakini pia neno linasema uushinde ubaya kwa wema.
Kila mahali nilipopita sijawahi kulipiza kisasi, na sitafanya hivyo! Mnichunguze ninachoongea na ninachohubiri mtagundua niko hivyo. Familia yangu iko hapa na itathibitisha kwamba ndivyo nilivyo.
Nendeni popote hata mpaka shule ya msingi na sekondari niliposomea, watawaambia hivyo hivyo. Hata vyuo vikuu nilivyosoma niko hivyo hivyo, “I am just like that!” Nimeshawahi kuitwa “Appologetic man” na wazungu kwa sababu ya kutubu kila wakati, [pamoja na kwamba mimi siyo mtu (man)], na sijawahi kuwaza kulipa kisasi, mnitambue hivyo, na mnichunguze mtakuta niko hivyo!
Kwa hiyo leo uamue kama unataka kwenda mbinguni uende, kama unataka kubali ubaki!
Hata nyumbani kwangu nikiona mtoto anataka kumuadhibu mwingine huwa nakuwa mkali, kwa sababu mtoto hajui kumuadhibu mwenzake ila mzazi ndiye ana uwezo wa kumuadhibu mtoto.
Ukilipa kisasi MUNGU anakuacha, hakutetei; Je! wewe hutaki kutetewa na MUNGU? Ndiyo maana jana niliamka na Neno moja niliposikia kijana mmoja anataka kwenda mahakamani kwenda kuwashtaki walionitukana. Nikasema hapana, msifanye hivyo mtakuwa mmemsaidia MUNGU, na MUNGU hasaidiwi. Hata hapa ninapofundisha si kwamba namsaidia MUNGU, yeye anajitosheleza na vitu vyote ni watumishi wake. Leo kuna majira ya aina yake ambayo tunaisimamisha, muelewe hivyo. Haijawahi kutokea hii majira, mnifahamu kabisa. Kwa hiyo mnapokuja kunisimulia kwamba fulani kaniudhi, huwa nawaangalia, mimi nataka uje kuniambia kwamba nimetubu leo kwa ajili ya fulani, vinginevyo huwa navumilia tu natamani nikuulize maswali lakini huwa nakuvumilia tu ili nisije nikakutoa kwa “rato”.
3. Isa.33:6 - Nasubiri majira ya jambo husika
Hapa nina maana kwamba, kama naishi kwa msingi wa Neno halafu silipi kisasi, huwa kunakuja mtihani wa kusubiri majibu. Kutojitetea, wale walioko karibu na wewe wasiomjua MUNGU, huwa, wanadhani kwa kuwa hukujitetea basi umefanya jambo hilo, na kwa sababu hiyo unaona aibu. Nafsi ya mtu ndivyo inavyokuwa, maana watasema, “unaona sasa, ametubu, amefanya”.
Hiyo hata nyumbani kwangu huwa nawaambia msijetetee, wananiambia watasema tumefanya, mimi nawaambia acha waseme lakini baada ya wiki moja itajulikana kwamba hatujafanya! Sasa, kusubiri hiyo wiki moja ipite usemwe vibaya ili baadaye uje usemwe vizuri huwa inakuwa kazi.
Ushuhuda:
Nina binti anayeitwa Uweza mtoto wa ndugu wa unabii, alikuwa analalamika, katika kusubiri wiki ipite ili waseme, vizuri. Kwa hiyo wakianza kusema alikuwa anasema baba, sasa ona tegeta nzima inasema mimi ndiyo nimefanya! Ndiyo sasa hivi na yeye amekuja kunielewa.
Ufahamu:
Je! utakuwa unasubiri wiki moja ili waje kuthibitisha kwamba hukufanya ili baadaye wakuseme uko sahihi? Mimi nimekubali kwanza, waniseme, ni tapeli, zulumati. Lakini hatimaye MUNGU amekuja kunisafisha, kwa sababu nimesubiri majira; bila kusubiri majira:
+ Kanisa lisingepona;
+ Jamii isingepona kwa sababu, kumbuka kwamba si swala tu la Kanisa, ila ni dunia nzima inaona wivu kwamba kwa nini Tanzania iitwe taifa la MUNGU?
+ Taifa lisingepona,
+ Uumbaji wote usingepona.
Katika kuangalia majira ni lazima uangalie uko wapi? Je! Wewe, uko tayari kutukanwa kwa muda mfupi ili upate ile faida kubwa itakayotokea? Maana hilo la kusubiri ndilo ambalo linasababisha ukunje ngumi, sikubali! Sikubali! Siwezi kuonewa mimi, naenda mahakamani!
Faida ya kusubiri majira:
Ukisubiri majira, Neno linasema katika Isa 33:6 “nyakati zako zitakuwa nyakati za kukaa imara; za wokovu tele; hekima na maarifa, kumcha BWANA ni hazina yake ya milele” kila mmoja atagundua kuwa una hekima, ila haiji siku ile ile. Haionekani siku hiyo hiyo!
Mmeona mimi nilivyosubiri na majibu yaliyokuja. Binti uliyekuwa umechumbiwa ukaachwa, usilie, kuna kitu MUNGU amekuepusha. Subiri majira MUNGU ili aje mzuri zaidi ya yule ambaye MUNGU amekuepusha naye. Lakini sharti usubiri. Naishi hivyo narudia nichunguze, na kama MUNGU hajaniambia sikuambii kitu, wala sitaona aibu kwamba atasema sina upako, ni mpaka MUNGU aniambie
4. 2Nya.7:14-16 – Naishi Toba na Unyenyekevu
Wale wanaosema mimi ni “dictator” (mbabe) huwa nashangaa! Mimi sijui ubabe wangu uko wapi, labda kwa sababu huwa nasubiri MUNGU aseme. Sijawahi kupiga ngumi yeyote, labda ngumi ya rohoni. Lakini hii ngumi ya mkono, hata mtoto wangu wa viungo vya ufunuo anaweza kusema.
Hata Neno linasema kwamba, ikiwa watu watajinyenyekesha na kutubu (kumbe anayetakiwa kufanya toba ni aliyeitwa kwa jina la MUNGU), toba yake huyo huwa inasikika. Toba ya muovu haisikiki bali toba yako wewe mwenye haki inasikika na inaonekana; kwa hiyo ukinigusa tu MUNGU hakawii.
Wengine wanasema nimekataa kuitwa mzee wa toba lakini nitawaeleza. Katika 1Fal.20:41-42, kwa nafasi yangu kuna kitu kimebadilika, na ndiyo maana mara nyingi nawaambia muende kwa NJIAZABWANA, kwa sababu kuna mamlaka MUNGU amempa.
Ukisoma hapo utaona kwamba kuna Nabii mmoja aliyemhurumia mfalme aliyehukumiwa na MUNGU, MUNGU akamwambia, “wewe nabii, kwa kuwa, umemhurumia yule niliyemhukumu, roho yako inakuwa badala ya huyo mfalme na watu wako badala ya watu wake, yaani wote unaofuatana nao, watalipuliwa, badala ya watu wake”.
Kwa hiyo, sasa hivi, mimi nikimhurumia yeyote, kwa toba aliyehukumiwa na MUNGU, maana yake mimi nife na ninyi wote. Je! hiyo ni sawa? Mwenye matatizo aende kwa MUNGU moja kwa moja. Unajua wengi hamtaki nihame vituo, mnataka niendelee kuwa Kuhani Kiongozi na NJIAZABWANA mnataka aendelee kuwa Mkuu wa Njia ya Magharibi.
Nimehamishwa kituo, sasa hivi hata zile certificates za maagano sisaini mimi, anasaini NJIAZABWANA, hata barua zote anasaini yeye siyo mimi. Anayetakiwa kuwa Kuhani Kiongozi ni yeye siyo mimi. Mimi namfunika kila mmoja. Narudia tena kusema kwamba, mimi nikimhurumia aliyehukumiwa na MUNGU natafuta balaa. Ikiwa MUNGU akisema huyu afe, halafu mimi nikasema asife, MUNGU anasema mimi nife na wakati nimembeba yeye na Kristo. Halafu na ninyi, je! hiyo ni sawa? Je!
· Niue kizazi ?
· Niue Taifa ?
Kwa hiyo mkisema nimekataa kuitwa Mzee wa Toba ni sawa? Hilo la Mzee wa Toba limehamia kwa NJIAZABWANA! Ingawaje sijaacha toba, lakini si kwa aliyehukumiwa na MUNGU, mimi naruhusiwa kutubu kwa ajili ya aliyehukumiwa na shetani, ibilisi, joka na kerubi, lakini aliyehukumiwa na MUNGU, siruhusiwi! Maisha ya toba bado yako pale pale; ila siyo kwa ajili ya aliyehukumiwa na MUNGU. Nikifanya hivyo, mimi nitakufa badala yake, na kanisa litakufa badala ya uumbaji wote, yaani nikifanya hivyo, nafufua behewa la nje, namfufua kahaba mkuu, nafufua mnyama, dunia, vyura watatu, joka, na vyote ambavyo tulivifuta. Hii ndiyo wiki ya ufahamu, na ndiyo maana mkimruka mtendaji wangu mnakosea, kwa hiyo nikifanya hivyo si kwamba sina upendo tena, ndiyo utii zaidi.
5. Kukaa kimya mpaka MUNGU aseme, Kut.14:14
Kukaa kimya siyo kiburi. Ukikaa kimya MUNGU anakupigania na kukutetea. “Ni kwa nini huwa mnakuwa na maneno mengi”?
Kila kukitokea jambo huwa kuna wanaokuja kusikiliza kama nalaani au natukana, mimi siwezi kufanya hivyo! Nimeitwa kwa ajili ya Neno tu! Nimeshasema silipi kisasi. Siruhusiwi kukuhukumu kwa sababu nitakuwa nimetumia mamlaka vibaya ambayo MUNGU amenipa.
Ninyi wenyewe mmesikia kwamba yeyote akinisingizia, chochote mimi huwa nanyamaza, ila usije ukafikiri kwamba MUNGU atakuacha! Hatakuacha ni lazima ashughulike na wewe! Ninyi hamkuelewa Eliya AD2 alikuwa anamaanisha nini aliposema huyu, msimguse, niguseni mimi ila huyu msimguse kwa sababu hamtasamehewa. Alijua, kwa sababu ninatetewa na MUNGU. Sasa wewe unataka maisha gani? Ya kutetewa na shetani, kichwa wako, Kanisa wako?
6. Kumtegemea MUNGU tu bila mchanganyo wowote - Hes.18:20
Neno linasema, kwamba, “Kisha BWANA akamwambia Haruni, “wewe hutakuwa na urithi, katika nchi yao, wala hutakuwa na fungu lolote katikati yao (Israeli) kwa sababu mimi ni urithi wako na fungu lako katika wana wa Israeli”. Kwa hiyo mimi ninavyojua fungu langu huwa liko kwa MUNGU. Hivyo unipe posho, usinipe, kila siku nitajipanga hapa foleni na nitafika hapa. Huyu aliyeniambia niache kila kitu kama ni kuaibika aaibike yeye. Mimi sijawahi kuomba msaada popote ingawaje kuna walioongea vitu vya ajabu sana. Kwamba zile fedha za madawati tumezipata UN?
7. Rum.8:28 – Mabaya au mema kwangu yote ni sawa
Kwa sababu najitambua nimeitwa kwa kusudi la MUNGU, hata lingekuja baya namna gani MUNGU ataligeuza liwe jema. Sikuitwa na pepo maana pepo kazi yake ni kuharibu. Nimeitwa na MUNGU hapa, kwamba utakamilisha kazi yangu, hilo ni kusudi la MUNGU. Kama nimeitwa nilikamilishe Kanisa siwezi kukusimamisha pale pale lazima nikuhamishe vituo. Sasa kukuhamisha vituo ni kosa? Sikuleta imani nyingine hapa! Mataifa yote yanakuja hapa lakini mataifa haya yote yana miungu yao, wakija hapa wakakuta MUNGU anaitwa kwa jina la Miaka1000 watamkubali? Maana na wao watasema na sisi tunaye.
· Wale waIsraeli na wao watakuja wakikuta tunasema MUNGU wa Ibrahimu, watasema kama ni wa Ibrahimu, wa Isaka, Yakobo, Paulo, na sisi tunaye. Lakini wakija tukawambia huyu ndiye aliyewatuma wote hao. Maana watajua kwamba huyu tuliye naye ndiye ametuma wote! Pamoja na yule aliyeleta Kizazi cha Nne.
· Bohora nao watasema tunaye, wahindu nao watasema tunaye. Lakini huyu Watampokea na Watasema huyo tunamtaka.
· Ukienda India kuhubiri wakati ule wa kizazi cha tatu, walikuwa wanakuuliza Yesu ni MUNGU wa nini, maana ninaye mungu wa fedha, ninaye mungu wa kupendwa, huyo kazi yake ni nini? Huyo atakuwa wa 10, je ni shilingi ngapi maana yake kila mungu ana kiwango chake.
Unaanza kujiuliza sijui nifanyeje ili wanielewe? Maana wana miungu mingi sana. Wale wanaowafahamu wanawajua, sasa huyu tuliye naye ndiye top, aliyetuma wote! Na Eliya aliponiambia nikamilishe, Kanisa alikuwa na maana kwamba niwahamishe pale alipotuacha niwapeleke mbele zaidi, sasa nimekosea wapi? Je! ni elimu nyingine au imani nyingine?
Kwa hiyo, huyu MUNGU ndiye atakayesababisha utimilifu wa Isa 2:2 . Kila mmoja, kila lugha, kila kabila, kila Taifa, litamjua huyu.
+ Wachina watakuja watauliza …tutawaambia siyo huyo!
+ Wajapani watakuja watasema sisi tunaye huyu, tutawaambia siyo huyo sisi tuna aliyetuma wote vizazi vyote.
+ ambao wangetusumbua zaidi ni waIsreali kwa sababu hao wote walioandikwa kwenye kitabu wangesema hawa wametokea kwetu, kwa hiyo tusingekuwa na kitu cha kuwaambia!
Ni lazima muelewa haya mambo:
+ Ukoo wa Musa wangekuja, ungewaambia nini?
+ Ukoo wa Yoshua pia; Eliya Mtishbi; Elisha; Daudi; Yesu; Petro; Paulo n.k.
Swali lao la kwanza wangeuliza ni kwamba huyu ni MUNGU wa Waha au, na wewe ungewajibu kwamba huyu ni MUNGU aliyetuma wote, vizazi vyote. Ndiyo maana nikakwambia useme vizuri, useme vibaya, najua MUNGU atageuza kwa sababu nimeitwa kwa kusudi lake, lakini ukianza kujitetea ina maana huna hakika naye.
8. Law.19:2 – uwe mtakatifu kama MUNGU alivyo.
HAWA NI WAKAMILIFU. |
Ukisema MUNGU wa Ibrahimu maana yake Ibrahimu yuko mbele na MUNGU yuko nyuma. Kadhalika MUNGU wa Isaka, Yakobo na wengine wote. Ndiko alikokuwa anaishi. Waovu wakitaka kuwasha kizazi, wanakaa kwa hilo jina ambalo MUNGU ametajwa kwalo.
Kulikuwa na siri ya ajabu sana lakini si kwamba walifahamu, na MUNGU aliruhusu kwa sababu ya majira. Mimi nimesema MUNGU aende mbele ili mimi nijifunze kwake, halafu nije nifundishe. Nimemuweka MUNGU mbele ili yeyote anayekuja akutane na yeye. Wengine wanasema mimi mchawi, sijui wanatoa wapi; ni MUNGU yuko mbele.
NIMEMALIZIA NILIPOANZIA, NIMEANZIA NILIPOISHIA!
Kwa namna hii utaniua ?
Wewe unatamani maisha gani ?
Kuna wanaosema watanifukuza; Utanifukuzaje na wewe hukunipaka mafuta ?
MIAKA 1000 YA KUTAWALA NA KRISTO WAKILI WA MUNGU KIZAZI CHA MUNGU |
UNA UWEZO WA KUKAA KWENYE KITI CHA MUNGU NA KUSEMA NINAMFUKUZA MIAKA1000 ?
KUINUA MAJIRA NA NYAKATI ZA KUISHI KAMA WAKILI WA MUNGU ANAVYOISHI!!!
No comments:
Post a Comment